2 Corinthians 12

Maono Ya Paulo Na Mwiba Aliokuwa Nao

1 aYanipasa nijisifu, ingawa haifaidi kitu. Nitaenda kwenye maono na ufunuo kutoka kwa Bwana. 2 bNamjua mtu mmoja katika Al-Masihi ambaye miaka kumi na minne iliyopita alichukuliwa juu hadi mbingu ya tatu. Kama ni katika mwili au nje ya mwili, sijui, Mungu ajua. 3Nami najua ya kwamba mtu huyu, kwamba ni katika mwili au nje ya mwili mimi sijui, lakini Mungu ajua, 4 calinyakuliwa hadi Paradiso.
Paradiso hapa ina maana mbinguni.
Huko alisikia mambo yasiyoelezeka, mambo ambayo binadamu hana ruhusa ya kuyasimulia.
5 eNitajisifu kwa ajili ya mtu kama huyo, lakini sitajisifu kuhusu mimi mwenyewe ila mimi nitajisifia udhaifu wangu. 6 fHata kama ningependa kujisifu, sitakuwa mjinga, kwa maana nitakuwa nasema kweli. Lakini najizuia, ili mtu yeyote asije akaniona mimi kuwa bora zaidi kuliko ninavyoonekana katika yale ninayotenda na kusema.

7 gIli kunizuia nisijivune kwa sababu ya ufunuo huu mkuu, nilipewa mwiba katika mwili wangu, mjumbe wa Shetani, ili anitese. 8 hKwa habari ya jambo hili nilimsihi Bwana mara tatu aniondolee mwiba huu. 9 iLakini aliniambia, “Neema yangu inakutosha, kwa kuwa uweza wangu hukamilika katika udhaifu.” Kwa hiyo nitajisifu kwa furaha zaidi kuhusu udhaifu wangu, ili uweza wa Al-Masihi ukae juu yangu. 10 jHii ndiyo sababu, kwa ajili ya Al-Masihi, nafurahia udhaifu, katika kutukanwa, katika taabu, katika mateso na katika shida, kwa maana ninapokuwa dhaifu, ndipo nina nguvu.

Wasiwasi Wa Paulo Kwa Wakorintho

11 kNimekuwa mjinga, lakini ninyi mmenilazimisha niwe hivyo. Kwa kuwa ilinipasa kusifiwa na ninyi, kwa sababu mimi si dhalili kuliko wale “mitume walio bora,” ingawa mimi si kitu. 12 lMambo yanayomtambulisha mtume wa kweli, yaani, ishara, miujiza na maajabu, yalifanywa miongoni mwenu kwa saburi nyingi. 13 mJe, ninyi ni kitu gani mlichopungukiwa kuliko makanisa mengine, ila tu kwamba mimi sikuwa mzigo kwenu? Nisameheni kwa kosa hili!

14 nSasa niko tayari kuja kwenu kwa mara hii ya tatu, nami sitawalemea, kwa sababu sitahitaji chochote chenu, ila ninawahitaji ninyi, kwa kuwa hata hivyo watoto hawaweki akiba kwa ajili ya wazazi wao, bali wazazi huweka akiba kwa ajili ya watoto wao. 15 oHivyo nitafurahi kutumia kila kitu nilicho nacho kwa ajili yenu, hata mwili wangu pia. Hata ingawa inaonekana ninavyozidi kuwapenda, ndivyo upendo wenu kwangu unavyopungua. 16 pIwe iwavyo, kwa vyovyote vile mimi sikuwalemea. Lakini kwa mimi kuwa mwerevu naliwapata. 17 qJe, nilijipatia faida kwa kumtumia mtu yeyote niliyemtuma kwenu? 18 rNilimshawishi Tito aje kwenu, nami nilimtuma pamoja na ndugu yetu. Je, Tito aliwatumia ninyi ili kujipatia faida? Je, hatuenendi kwa roho moja, na hatuchukui hatua zile zile?

19 sJe, mmekuwa mkifikiri kwamba sisi tunajaribu kujitetea mbele yenu? Sisi tumekuwa tukinena mbele za Mungu kama wale walio katika Al-Masihi. Na chochote tufanyacho, ndugu wapendwa, ni kwa ajili ya kuwatia nguvu. 20 tKwa kuwa nina hofu ya kwamba nitakapokuja naweza kuwakuta nisivyotaka, nanyi mkanikuta msivyotaka. Nina hofu kwamba panaweza kuwa na ugomvi, wivu, ghadhabu, fitina, masingizio, masengenyo, majivuno na machafuko. 21 uNina hofu kwamba nitakapokuja tena kwenu, Mungu wangu atanidhili mbele yenu, nami nitasikitishwa na wengi waliotenda dhambi mbeleni, na wala hawajatubu kwa uchafu wao, uasherati, na ufisadi walioushiriki.
Copyright information for SwhKC